MKAPA AONGOZA HARAMBEE KUCHANGIA MFUKO WA UDHAMINI KUDHIBITI UKIMWI
RAIS Mstaafu Benjamin Mkapa amewataka wadau mbalimbali na wananchi kuendelea kuchangia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo nchini ambapo zaidi ya sh.milioni 200 zilipatikana.
Mkapa alitoa ombi hilo wakati akiongoza harambee ya kuchangia mfuko huo iliyofanyika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya nje na ndani pamoja na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.
"Ni wajibu kwa kila mwananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuchangia mfuko huu ili kusaidia mapambano ya Ukimwi hapa nchini na kuwa mapmbano hayo si ya mtu mmoja" alisema Mkapa. Katika hatua nyingine Rais Mstaafu Mkapa ameiomba Serikali kuendelea kutenga fedha za Ukimwi katika bajeti zake.
Akizungumza katika harambee hiyo Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama alisema kwamba Serikali itaendelea kusimamia Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) katika matumizi ya fedha hizo.
Mhagama alisema asilimia 60 ya fedha hizo zitatumika kununulia madawa, asilimia 25 itatumika katika kutoa huduma za kinga pamoja na kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya Ukimwi na asilimia 15 zitatumika kwa ajili ya uwezeshaji na ufuatiliaji wa programu za Ukimwi.
Comments
Post a Comment