sunzua

Maambukizi ya virusi vya papilloma (HPV) 


By Dk Isaack Maro
Virusi hivi vikoje?
Virusi vya papilloma ni miongoni mwa virusi hatari duniani vinavyoweza kusababisha maradhi  ya zinaa.
Virusi hivi husababisha maradhi ya zinaa yaliyoenea zaidi ulimwenguni kuliko maradhi mengine yanayosababishwa na vimelea vya aina nyingine.
Kuna zaidi ya aina 40 za virusi hivi vya human papilloma ambavyo vina uwezo wa kudhuru maeneo ya siri ya wanaume na wanawake.
Virusi vya papilloma vinaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya ukiachilia mbali yale ya kwenye ngozi pekee.
Wengi wetu tunaweza kuwa na virusi hivi, lakini tukaishi muda wote wa maisha yetu bila virusi hivi kusababisha tatizo lolote.
Lakini, kwa baadhi yetu  wao hupata matatizo ya kiafya tena makubwa kutokana na maambukizo ya virusi hivi.
Virusi hivi ni tofauti na virusi vya hepesi (Herpes) wala virusi vya Ukimwi (VVU)
Virusi vyote hivi vinaweza kuambukizwa kwa njia ya ngono isiyo salama, lakini tofauti yao iko kwenye namna maradhi yatokanayo na uambukizi wake yanavyojitokeza mwilini.
Nani yuko hatarini kupata maambukizi?
Mtu yeyote ambaye anashiriki ngono yuko kwenye hatari ya kupata maambukizi ya virusi hivi vya  papilloma.
Virusi hivi vimeenea zaidi ulimwenguni, hivyo ni rahisi sana kwa mtu kuvipata pale atakaposhiriki ngono.
Hii inawezekana kabisa hata kwa wale wenye mpenzi mmoja.
Maambukizi yake
Virusi vya papilloma huambukizwa kwa njia ya ngono hasa isiyo salama. Ninapozungumzia ngono hapa ninamaanisha aina zote za ngono ikiwemo ya kinyume cha maumbile.
Virusi hivi vinaweza kuambukizwa hata kama aliyenavyo hana dalili yoyote ya maradhi yatokanayo na virusi alivyokuwa navyo.
Watu wenye maambukizo ya virusi hivi huweza kuambukizana wenyewe miaka kadhaa tangu wao walipoambukizwa bila kuonyesha dalili yoyote ya madhara.
Mara chache sana hutokea mama mjamzito akamwambukiza mtoto wake virusi hivi wakati wa uzazi (kujifungua)
Idadi kubwa ya wale wanaopata maambukizi ya virusi vya papilloma hawaonyeshi dalili zozote za maambukizi ya virusi hivi.
Pia, huwa hawapati maradhi yanayosababishwa na maambukizi ya virusi hivi. Mara nyingi maradhi yanayosababishwa na virusi hivi huwa yanatoweka yenyewe bila matibabu ya aina yoyote katika kipindi cha miaka miwili (2) hadi minne (4) tangu uambukizi.
Kwa wale ambao wanapata maambukizi na baadaye kupata maradhi yanayotokana na maambukizi wanaweza kupata magonjwa kati ya yafuatayo;
Sunzua, saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya maumbile ya kiume na kike.
Pia, maambukizi ya virusi hivi yanaweza kusababisha mtu kupata matatizo ya mapafu ambako sunzua huota kwenye mapafu na kuleta matatizo kwenye mapafu na mfumo wa upumuaji.
Hata hivyo, aina ya virusi vinavyosababisha sunzua ni tofauti na ile inayosababisha saratani.
Sunzua(warts) ni ugonjwa wa ngozi unaofahamika na wengi. Ugonjwa huu husababishwa na virusi ambavyo kitaalamu huitwa human papilloma virus.
Karibu asilimia 10 ya wanadamu wamewahi kupata athari za virusi vya ugonjwa huu, achilia mbali kuumwa sunzua.
Kwa sababu hiyo ndiyo kusema kila mtu anapaswa kufahamu ugonjwa huu kwa undani ili unapojitokeza awahi hospitali ili kuudhibiti.
Virusi vinavyosababisha ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya ngono.
Ugonjwa huu hutokea sehemu mbalimbali za mwili, lakini huwatokea wengi sehemu za siri.
Sunzua kama ugonjwa wa zinaa, huathiri sehemu za siri pamoja na njia ya haja kubwa.
Wagonjwa ambao wanaishi na Virusi vya Ukimwi wako kwenye mazingira hatarishi zaidi ya kupata sunzua.  
Virusi vinavyosababisha maradhi ya sunzua huambukizwa kwa njia ya ngono na ni mara chache huweza kusambaa kwa njia ya kugusana.
Virusi wa maradhi haya wanajulikana kama papilloma na hujitokeza kwenye eneo la ngozi ambapo virusi hivi vimepenya. Mara nyingi hujipachika kwenye mchubuko au mpasuko wa ngozi.
Maradhi haya huweza kujitokeza kwenye ngozi kati ya miezi miwili hadi tisa baada ya kupenya kwenye ngozi.
Maradhi haya husababisha ngozi kutokuwa na muonekano wake wa kawaida.
Husababisha ngozi kuwa na milima na mabonde kiasi cha kusababisha kukatika kwa urahisi na kufanya virusi kuendelea kupenya.
Dalili za maradhi haya ni kuwa na ngozi iliyoinuka, iliyopoteza unyoofu wake na yenye muonekano mfano wa maua.
Sunzua ziko za aina tofauti kulingana na mahali ugonjwa unatokea na kuonekana kuiathiri ngozi.
Sunzua ya sehemu za siri au kwa kitaalamu condyloma acuminatum (venereal warts).
Aina hii ya ugonjwa kwa wanawake huathiri sehemu za nje za maumbile ya siri na mara nyingine huweza kujitokeza na kuathiri shingo ya kizazi.
Kwa wanaume sunzua huathiri uume wenyewe, korodani, nyonga mpaka kwenye mapaja.
Sunzua hii ya sehemu za siri kwa watu wa jinsia zote hujitokeza kama uvimbe ulioinuka au zikawa sawia bila uvimbe wa aina yoyote.
Sunzua zinaweza kuwa kubwa au ndogo, zikawa mojamoja au zikajikusanya pamoja kama mafungu zikafanana kabisa na maua.
Huwa zinaweza kutokea usoni, hasa sehemu karibu na kope ama maeneo mengine kama vile vidole vya miguu na mikono.
Sunzua huwa haziumi na sanasana huwa zinawasha na huweza kujitokeza katika kipindi cha miezi miwili mpaka tisa baada ya maambukizi ya virusi.
Kwa wanawake, sunzua ya kwenye shingo ya kizazi huweza kusababisha saratani ya shingo ya kizazi.
Kwa sababu hiyo, mwanamke anapaswa kujichunguza ili kuchukua hatua mwafaka za matibabu.
Ndugu msomaji, kwa jumla magonjwa ya ngozi ni mengi na yanaathiri binadamu kwa namna tofauti. Kama nilivyoeleza hapo awali, yanayotokana na bakteria, fangasi, virusi na hitilafu nyingine katika damu au ngozi.
Tutaendelea kujibu maswali mbalimbali ya wasomaji kulingana na mtakavyouliza. Kwa wale ambao maswali hayakujibiwa wasikate tamaa kwani kadri tutakavyopata nafasi, yataendelea kujibiwa.

Comments

Popular posts from this blog